Pages

Sample Text

Frank Kimaro run this blog

11/15/2011

Kama kawaida Lema apokelewa kwa kishindo Arusha, baada ya kutoka jela.


SHUGHULI mbalimbali za kibiashara na kijamii katika Jiji la Arusha jana zilisimama kwa muda kupisha mapokezi ya Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema baada ya kutoka rumande katika Gereza la Kisongo alilokaa kwa siku 14.Oktoba 31, mwaka huu, Lema na wenzake 18 walifikishwa mahakamani wakidaiwa kufanya kusanyiko lisilo halali na kukaidi amri ya polisi iliyowataka watawanyike yeye na wenzake.
Walikamatwa na kufikishwa mahakamani na kudhaminiwa lakini Lema akikataa dhamana akisema ameamua kutangulia gerezani kudhihirisha kwamba haogopi gereza.Lema alitoka kwa dhamana na kuandaliwa mapokezi makubwa ya wafuasi wa Chadema ambayo yaligeuka kuwa maandamano ya amani.Shamrashamra za mapokezi hayo zilisababisha kusimama kwa muda kwa shughuli kadhaa kama huduma za kibenki hasa zile zilizo katika Barabara ya Sokoine.

Wakati wa maandamano hayo wafuasi hao wa Chadema walikuwa wakipeperusha majani na matawi ya miti.
Mahakimu, mawakili na makarani wa mahakama nao walilazimika kuacha shughuli zao kwa muda na kutoka nje kushuhudia mapokezi ya mbunge huyo yaliyokuwa yakipambwa kwa nyimbo mbalimbali nje ya mahakama hiyo.

Sehemu ya nyimbo hizo zilimgusa Mkuu wa Polisi Wilaya hiyo ya Arusha, Zuberi Mwombeji ambaye hivi karibuni aliingia kwenye mvutano mkubwa na chama hicho cha upinzani akituhumiwa kutumia nguvu kuwadhibiti viongozi wake.Waliimba: “Tunamtaka….panya wetu… tunamtaka mbunge wetu… Zuberi (OCD), aondoke. Mlituvizia usiku, leo sasa ni mchana hapatatosha. Hatuandamani, tunampokea shujaa wetu.”

Shamrashamra hizo pia ziliambatana na mabango mbalimbali huku pia kukiwa na fulana maalumu zilizokuwa zimevaliwa na baadhi ya mashabiki zikiwa na maneno yaliyosomeka: “Lema kaonyesha njia mbadala ya kudai haki. Jela ni mahali pa kuishi kama sababu ya kwenda huko ni vita
dhidi uonevu, ukandamizaji wa haki na utu wa binadamu.”

Mahakamani
Lema aliyefika mahakamani Saa 3:20 asubuhi akiwa ndani ya gari maalumu ya polisi, alipewa dhamana na Hakimu Mkazi, Judith Kamara baada ya kukamilisha masharti ya kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho na barua za utambulisho ambao walisaini hati ya dhamana ya Sh5 milioni kila mmoja.

Alidhaminiwa na Sarah Mohamed na Mwajuma Manonge na kutoka eneo la Mahakama Saa 5:15 asubuhi akiwa amebebwa juujuu na wafuasi wake baada ya juhudi zake za kutaka kuondoka kwa kutumia gari lake kushindikana.Wafuasi hao walimzuia kuingia katika gari lake na kumtaka atembee kwa miguu hadi eneo la Ngarenaro ziliko Ofisi za Chadema Mkoa wa Arusha.
Mbunge huyo hakuwa na budi kukubaliana na agizo hilo la wafuasi wake kuongozana hadi Ngarenaro lakini aliwasihi wamruhusu apande na kusimama juu ya gari lake, ombi lililokubaliwa.

Licha ya mashabiki hao wa Chadema kulazimisha kumbeba Lema juujuu na kuanza kutoka naye eneo la Mahakama huku wakiimba, Kamanda wa Operesheni Maalumu za Polisi Mkoa wa Arusha, Peter Mvulla aliwaamuru askari wake waliokuwa wakilinda amani eneo hilo kutowaingilia.

“Waacheni waandamane na mbunge wao, msiwapige mabomu. Subirini tuangalie kitu gani kitatokea. Kama hawafanyi vurugu msiwaingilie hadi nitakapotoa amri nyingine. Muhimu hakikisheni mmejipanga sawasawa kila eneo,” alisikika Mvulla akitoa maelekezo kwa simu.
Busara za Mvulla aliyekuwa mkuu wa kikosi cha ulinzi katika shughuli ya jana, zilisaidia kuepusha vurugu katika mapokezi hayo yaliyoishia kwa Lema kuwahutubia wafuasi wake nje ya ofisi za chama hicho mkoa huku amani na utulivu vikitawala.

Mkutano hadhara
Akihutubia umati mkubwa wa watu nje ya ofisi hizo, Lema alisema Serikali isidhani kuwa ina uwezo kutumia dola kusaidia CCM Arusha na kuonya kwamba, yuko tayari kujiuzulu nafasi yake ili kuruhusu uchaguzi mdogo akiahidi kunyakua tena kiti hicho kwa kura zaidi ya 56,196 alizopata kwenye uchaguzi uliopita.

“Maisha yangu siyo kwa ajili ya kuishi leo, bali kufa kwa faida. Ndiyo maana kila siku nasema ni heri vita inayotafuta haki, kuliko amani inayopumbaza na kudhalilisha utu wa mtu,” alisema huku akishangiliwa.Alisema jana usiku alipanga kuelekea Dodoma kuhudhuria kikao cha Bunge kushiriki mjadala wa Katiba Mpya akionya kuwa iwapo kutakuwapo uchakachuaji ataanzisha balaa jingine kubwa kuliko la Arusha.

Amjia juu RC
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya maandamano hayo, Lema alisema suluhu ya mgogoro wa Arusha utapatikana kwa uchaguzi wa umeya kurudiwa na kumuonya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo kuacha kudandia gari asilojua linakoelekea akimaanisha mgogoro unaoendelea.
“Bila haki kupatikana, sasa tutaanza maandamano kwenda majumbani mwa viongozi wanaokandamiza haki zetu. Waandae risasi na mabomu ya kutosha kwani mapambano ndiyo kwanza yameanza. Eti RC anauliza kwa nini hatuandamani sehemu nyingine, tukaandamane sehemu kama Tabora ambako hakuna sababu ya kufanya hivyo? Arusha tuna sababu ya kuandamana,” alisema Lema.

Kuhusu kauli aliyodai ya vitisho kutoka kwa Mulongo aliyeonya wanaopanga kuvuruga amani na utulivu Arusha, Lema alisema kiongozi huyo bado anakabiliwa na ugeni ndiyo sababu anatoa kauli bila kuzifanyia utafiti.

Jiji la Arusha limekuwa likigubikwa na vurugu za kisiasa mara kwa mara tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambao pamoja na mambo mengine, uliacha majeraha yanayotokana na matokeo ya uchaguzi wa umeya ambao Chadema umekuwa ukiyapinga.

No comments:

Post a Comment

COMMENT HAPA UKIMALIZA, KWENYE PROFILE SELECT ANONYMOUS KISHA BONYEZA PUBLISH.