Katika kauli hiyo, Makinda anadaiwa kunukuliwa na vyombo vya habari akisema wabunge wa Chadema hawakuwatendea haki wananchi waliowatuma bungeni kutokana na uamuzi wao wa kususia mjadala huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu wa Wabunge wa chama hicho, John Mnyika, alisema Spika Makinda siyo msemaji wa wapiga kura wao na amemtaka ashughulike na wapiga kura wa jimbo lake la Njombe Kusini.
Mkutano huo, ulihudhuriwa pia na Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu.
“Tumetafakari hoja zinazoendelea kujengwa kwamba wabunge wa CHADEMA hawakuwatendea haki wananchi waliowatuma kuwawakilisha bungeni kutokana na uamuzi wetu wa kususia mjadala wa Katiba.
“Tunamtaka Spika ajue yeye si msemaji wa wapiga kura wetu, waliotuchagua wanatuamini na wanatupigia simu kwamba wanakubaliana na uamuzi wetu.
“Kama tungekubali muswada usomwe kwa mara ya pili, ingekuwa hatujawatendea haki wapiga kura wetu, lakini uamuzi wetu huu ndiyo msimamo wa wananchi katika suala hili, Spika ashughulike na wapiga kura wa jimbo lake,” alisema Mnyika.
Mbali na hilo, Mnyika pia alimgeukia Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila na kupinga kauli iliyotolewa na kiongozi huyo wa Bunge jana kupitia vyombo vya habari.
Katika maneno hayo, Dk. Kashilila anadaiwa kupinga uamuzi wa wabunge hao na kusema walipaswa kutumia kanuni ya 86 ya Bunge inayoruhusu mbunge kutoa hoja ya kuliomba Bunge au mjadala wa siku husika uahirishwe badala ya kususia.
“Tulimsikia Kashilila akisema tumeshindwa kutumia kanuni ya 86 (3) inayoruhusu mbunge kutoa hoja ya kutaka mjadala uahirishwe.
“Kauli hii inatoa picha kuwa, Kashila ametumwa na CCM au Serikali kufanya propaganda, Kashilila anatakiwa kufanya kazi yake ya kitaalamu au ya kiutendaji kama kiongozi wa mhimili wa Bunge.
“Kashilila ni mwongo, mimi nilisimama mara tatu nikitumia kanuni hiyo hiyo ya 86 kuomba mjadala uahirishwe, lakini Spika alininyima fursa wala hakutaka kuwauliza wabunge, akaangalie taarifa rasmi za kumbu kumbu za Bunge,” alisema Mnyika.
Katika hatua nyingine, Mnyika alisema Kamati Kuu (CC) ya chama chake itakutana Novemba 20, mwaka huu kujadili Muswada wa Katiba mpya ili kupanga utaratibu wa kwenda kwa wananchi.
Hata hivyo, Mnyika alisema wabunge wote wa Chadema watashiriki mkutano huo bila kujali ni wajumbe au laa na kwamba kutokana na kikao hicho baada ya Bunge kuhitimishwa Ijumaa wiki hii, wabunge wote wa chama hicho hawatashiriki shughuli nyingine za Bunge ikiwamo semina ya Jumamosi.
“Kwa maneno hayo ndiyo kusema kwamba, Jumamosi asubuhi wabunge wote wa CHADEMA tutaelekea Dar es Salaam kwa ajili ya kikao hicho kitakachofanyika siku ya Jumapili,” alisema.
Wakati huo huo, mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba jana uliendelea, ambapo baadhi ya wabunge walituhumu baadhi ya mabalozi na wafadhili kwamba wanashirikiana na wanaharakati na wanasiasa kutaka kuvuruga nchi.
Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM), ndiye aliyewashambulia mabalozi hao, akisema kuwa, wapo baadhi ya mabalozi hapa nchini ambao hawana nia njema na Watanzania.
“Hawa mabalozi wanatakiwa kutambua kwamba, wanatakiwa kuwaachia Watanzania waamue mambo yao yakiwamo haya ya kupata Katiba mpya pindi mchakato utakapoanza.
“Kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya mabalozi wanaonekana kushirikiana na baadhi ya wanasiasa na wanaharakati kwa nia ya kuhakikisha amani iliyopo inatoweka jambo ambalo Serikali inatakiwa kuwa makini,” alisema Ndassa.
SAID MTANDA
Mbunge wa Mchinga, Said Mtanda (CCM), pamoja na mambo mengine, alitumia fursa hiyo kutoa angalizo kwa Serikali kuwa makini na baadhi ya wanaharakati ambao wanaonekana kukosa dhamira nzuri.
Mtanda alionyesha wasiwasi kwa wanaharakati hao huku akisema wapo baadhi ya wafadhili kwa masharti yanayolenga kuwagawa Watanzania.
“Hao wanaharakati ndiyo ambao wamekuwa wakitoa mawazo hasi kwa Watanzania, baadhi ya wafadhili hawa wanatumia nafasi yao kufadhili baadhi ya wanaharakati kwa ajili ya kufanikisha mitazamo na malengo,” alisema Mtanda.
ANDREW CHENGE
Mbunge wa Bariadi Magharibi, Endrew Chenge (CCM), alisema kazi inayofanywa na wabunge kwa sasa ni sawa na kujenga barabara na kwamba kazi hiyo itafanikisha mchakato wa kupatikana Katiba mpya.
Chenge, aliwapiga vijembe wabunge wa CHADEMA, akisema ni jambo la kusikitisha kuwa baadhi ya kikundi cha watu wakijifanya wao ndiyo wana mawazo yanayofaa kuliko wengine.
Mjadala wa muswada ambao kwa mujibu wa ratiba ya Bunge ulikuwa uhitimishwe jana, umesogezwa mbele ambapo unatarjiwa kuendelea tena leo. Kwa mujibu wa Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani, hatua hiyo ni kutokana na ongezeko la wabunge kutaka kuuchangia.
BAVICHA YAKUNJUA MAKUCHA
Katika hatua nyingine, Baraza la Taifa la Vijana la CHADEMA (BAVICHA), limetangaza kupambana na wabunge wa CCM, wanaounga mkono Muswada wa Katiba mpya kusomwa bungeni kwa mara ya pili.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa BAVICHA, John Heche, alisema chama chake kiko tayari kupambana hadi kufa kwa ajili ya kuwatetea Watanzania na sasa wanaanza kazi ya kuzunguka katika majimbo ya wabunge wa CCM walionekana kutetea muswada huo ingawa umepingwa na vikali na wanaharakati.
“Muswada uliosomwa juzi kwa mara ya pili ni batili, kwa kuwa ulipaswa usomwe kwa mara ya kwanza, sasa tutaangalia wabunge wote ambao wameonekana kuuunga mkono, hao ndiyo tunaanza nao kwa kuzunguka kwenye majimbo yao kuhamasisha vijana na wafuasi wetu wakatae sera zao na udhalimu unaofanywa na Serikali ya CCM.
“Muswada uliosomwa kwa mara ya pili bungeni ni mbovu kuliko hata ule wa kwanza kwani baadhi ya mambo yameongezwa, mambo kandamizi yote yaliyokuwa kwa mara ya kwanza hayakuondolewa.
“Kitendo cha kulazimishwa kusomwa kwa mara ya pili, ni ujanja ujanja wa Serikali ya CCM na maswahiba wao, wenye nia ya kutaka kuzalisha Katiba itakayolinda maslahi yao na siyo matakwa ya wananchi.
“Katika hili BAVICHA itatoa kazi wa Jeshi la Polisi kwani hivi sasa jeshi hilo limeonekana kutokuwa na kazi ya kufanya zaidi ya kupambana na wafuasi wetu pamoja na wafanyabiashara ndogo ndogo (Wamachinga).
“Jeshi la Polisi linaonekana halina kazi ya kufanya, wameshindwa kuwakamata watumuhiwa mbalimbali nchini, kazi yao kubwa imebaki kupambana na CHADEMA, tunasema tutawapa kazi ya kufanya kwani tutafanya maandamano makubwa kwa wakati mmoja tuone watajigawa vipi.
“Katika vurugu za Mbeya kuna askari polisi walitolewa maeneo mengine kwa ajili ya kuongeza nguvu, sasa haya maandamano yanayokuja sijui watajigawa vipi,” alisema Heche.
AWAONYA UVCCM
Katika hatua nyingine, Heche amemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Martin Shigela, kuacha kulinganisha vijana wa Chadema na UVCCM.
“Juzi juzi nilimsikia Shigela akihamasisha vijana wa UVCCM, kujitokeza kutulaani, tunapenda kuwaambia hatubabaiki kabisa, namuomba Shigela apange maandamano tukutane aone namna patakavyochimbika,” alisema Heche.
Kuhusu halmashauri zinaozoongozwa na Chadema, alizitaka zitenge maeneo ya wafanyabiashara ndogondogo ili wafanye biashara zao bila usumbufu.
No comments:
Post a Comment
COMMENT HAPA UKIMALIZA, KWENYE PROFILE SELECT ANONYMOUS KISHA BONYEZA PUBLISH.