Aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,Shamsi Vuai Nahodha. |
Peter Saramba, Arusha
MMOJA wa wanachama wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, anadaiwa kutoroka na zaidi ya Sh26 milioni za jumuiya hiyo zilizochangwa kwenye harambee iliyofanyika Mei 9, mwaka juzi na kuongozwa na aliyekuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shamsi Vuai Nahodha. Akizungumza kwa simu kutoka Mererani, Simanjiro, Mwenyekiti wa UVCCM wilayani humo, Kiria Laizer alithibitisha kuwa fedha hizo zilizochangwa kwa lengo la kutunisha mfuko wa maendeleo ya vijana Simanjiro ziliyeyuka muda mfupi baada ya harambee hiyo.
Katika harambee hiyo, Nahodha ambaye sasa ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alichanga fedha taslimu Sh2 milioni.
Ilielezwa kwamba wageni wawili waliohudhuria shughuli hiyo kwa mwaliko wa mtuhumiwa huyo ambao walitambulishwa ukumbini kuwa dada wa Rais Kikwete, walichangia 400,000.
Kwa mujibu wa kumbukumbu rasmi za shughuli hiyo, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Henry Shekifu ambaye sasa ni Mbunge wa Lushoto (CCM), alichangia Sh500,000.
Viongozi wengine waliohudhuria na kiasi walichochanga kwenye mabano ni Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Khalid Mandya (200,000), Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka (Sh1.5 milioni), na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Manyara, Lucas Ole Mukusi (Sh100,000).
Laizer alisema tukio la wizi huo limebaki kuwa kama mchezo wa kuigiza huku baadhi ya wanachama na viongozi wenzake wakimtuhumu hata yeye wakidhani alihusika kwa njia moja au nyingine.
“Baada ya mgeni rasmi (Nahodha) kunikabidhi mfuko wenye fedha usiku ule pale ukumbini, nilimwita (mtuhumiwa jina tunalo) na kumkabidhi mbele na wajumbe wawili wa kamati ya utekelezaji wilaya na tangu siku ile, sijawahi kumwona wala kupata mawasiliano naye,” alisema Laizer.
Aliwataja Wajumbe wa Kamati ya Utendaji walioshuhudia makabidhiano hayo kuwa ni Bonny Shongo na Paul Sipitet.
“Siku tatu baadaye tulimtafuta (mtuhumiwa), bila mafanikio na tulipompata kwa njia ya simu alidai yuko Mjini Arusha kwa shughuli binafsi lakini baada ya muda mfupi alitutumia ujumbe mfupi wa simu akitutaka kutafuta mtu mwingine (wa kujaza nafasi yake) kwani yeye ameondoka,” alisema Sipitet.
Katibu wa UVCCM wilayani humo, Mwanakombo Amiri alisema kwa simu hakuna kumbukumbu yoyote kwenye majalada ya kiofisi inayohusu kikao cha maandalizi wala fedha zilizopatikana kwenye harambee hiyo.
“Hakuna chochote kwenye faili kuhusu jambo hilo unalouliza. Kikao kilichopita cha kamati ya utekelezaji kilizungumzia suala hilo ingawa haikuwa moja ya ajenda. Ila kikao kijacho ambacho siwezi kukutajia kitafanyika lini hilo ni moja ya ajenda muhimu na tutatoa uamuzi kulingana na kanuni zetu,” alisema Mwanakombo.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, ambaye ni miongoni mwa waliotafuniwa fedha zao walizochangia alithibitisha ofisi yake kupokea taarifa za fedha za kuyeyuka kwake na kusema tayari ameziagiza ngazi husika (UVCCM), kuchukua hatua kulingana na kanuni na taratibu zao na pia kutoa taarifa polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe.
“Sisi kama Serikali, chama kikichukua hatua na kuwasilisha taarifa, nitaagiza polisi wachukue hatua za kisheria kwa kuchunguza na kumtia mbaroni mtuhumiwa. Nakushauri pia uwasiliane na katibu wa CCM wilaya ambaye ndiye mlezi wa jumuiya zote za chama ngazi ya wilaya,” alisema Mandya.
Mkuu huyo wa wilaya alisema baada ya ofisi yake kutopata taarifa za utekelezaji wa amri yake ya mhusika kuchukuliwa hatua hadi sasa, ameamua kuuandikia barua rasmi uongozi wa UVCCM na chama wilaya kudai utekelezaji wa agizo lake kutokana na wahusika kuonekana wazito katika jambo hilo.
Hata hivyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Simanjiro, Jamila Mjungu alikataa kuzungumzia suala hilo akisema UVCCM ni jumuiya inayojitegemea, yenye viongozi na wasemaji na kanuni za kutatua matatizo yao.
Uchunguzi wa kina umebaini kuwa mtuhumiwa huyo sasa ni diwani katika moja ya kata za Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma ambako aligombea na kushinda kwenye uchaguzi mkuu uliopita.
Katibu Mkuu wa UVCCM, Martin Shigela alisema ingawa jambo hilo halijaripotiwa kwake na uongozi wa wilaya ya Simanjiro, atafuatilia na kuhakikisha mhusika anachukuliwa hatua kulingana na kanuni za jumuiya hiyo na sheria za nchi bila kujali cheo, umaarufu wala nasaba yake na viongozi.
“Kwanza inawezekana mtuhumiwa ni tapeli mzoefu anayetumia jina la mheshimiwa Rais na familia yake kuwatisha
........................... Chanzo ni mwananchi...................................................................