Pages

Sample Text

Frank Kimaro run this blog

12/14/2011

Mitihani ya darasa la saba yachakachuliwa wizara husika imetangaza

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philipo Mulugo akitangaza matokeo ya Mtihani wa Darasa la Saba kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam (Picha na Zacharia Osanga)


WANAFUNZI 9000 WAFUTIWA MATOKEO, HATA WALE WATAKAOINGIA KIDATO CHA KWANZA KUPIMWA UWEZO WAO UPYA 
Gedius Rwiza na Raymond Kaminyoge 
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imetangaza matokeo ya mitihani ya darasa la saba ikieleza kuwa wanafunzi 9000 wamefutiwa matokeo kutokana na udanganyifu na hata wale ambao watapangiwa shule za sekondari wapimwa uwezo wao kabla ya kuanza masomo.  Akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo pamoja na mambo mengine, alisema kutokana na tatizo hilo, wanafunzi waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza mwakani, watapaswa kuchujwa upya.

“Baada ya udanganyifu kuongezeka mwaka huu,  tumeanzisha utaratibu huu ili kuwabaini wanafunzi wanaingia kidato cha kwanza wakiwa hawajui kuhesabu, kusoma wala kuandika,"alisema Mulugo. 
Mulugo alisema wanafunzi waliofutiwa mtihani huo ni 9,736 na utaratibu wa kuchuja wale waliochaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza utaanza rasmi Januari mwakani.  Kuhusu wanafunzi kudanganya, alisema Wizara imegundua kuwapo kwa aina nne za udanganyifu ikiwamo wanafunzi 94 kukutwa na majibu katika karatasi, rula na viatu.   

“Watahiniwa wanne walibainika kuandikiwa majibu ambapo ilionekana miandiko zaidi ya mmoja kwenye karatasi ya mtahiniwa  mmoja.  Wataalamu wa masuala ya maandishi wamethibitisha suala hilo,’’alisema Maugo na kutaja udanganyifu mwingine kuwa ni wanafunzi tisa kurudia darasa la saba kinyume na taratibu.  Alisema aina nyingine ya udanganyifu waliougundua ni kuwapo kwa wanafunzi 9,629  waliokuwa na mfanano  usio wa kawaida katika kukosea majibu ya maswali.

Manyara kinara wa kuchakachua
 Waziri Mulugo alisema Mkoa wa Manyara ndio unaoongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya wanafunzi waliofutiwa matokeo. Alisema Mkoa huo una wanafunzi 1, 573 waliofutiwa matokeo, ukifuatiwa na mikoa ya Arusha (1,012) na Lindi (63).  

Akizungumzia kiwango cha ufaulu, Waziri Mulugo, alisema mwaka huu kimeongezeka kwa asilimia 4.76. Kiwango kimepanda hadi asilimia 58.28 kutoka asilimia 53 .52 ya mwaka jana. Mulugo alisema wanafunzi waliofanya mtihani huo walikuwa 983,545 na waliofaulu ni 567,567.  "Wasichana waliofaulu ni  278,377  sawa na asilimia 54.48  na wavulana ni 289,190  sawa na asilimia 62.49," alisema. 

Waziri Mulugo alisema katika kundi la wanafunzi wenye ulemavu, waliofaulu ni 355, kati yao wasichana ni 159 sawa na asilimia 44.79 na wavulana  196 sawa na asilimia 55.21.  Waliochaguliwa  kidato cha kwanza  Waziri Mulugo alisema  kati ya wanafunzi 567,567 waliofaulu,  wanafunzi 515,187 sawa na asilimia 90.1,  wamechaguliwa  kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za Serikali huku na 52,380 hawakupata nafasi.  "Wasichana waliochaguliwa ni  253,402 sawa na asilimia 49.1 na wavulana  261,785 sawa na asilimia 50.9," alisema. 

Ufaulu kwa kila somo  Mulugo alisema kuwa viwango vya ufaulu katika masomo ya Kiingereza, Hisabati na Sayansi, vimeongezeka ikilinganishwa na matokeo ya mwaka jana. "Kiwango  cha ufaulu kwa somo la  Kiingereza kimeongezeka kwa asilimia 10.23 kutoka asilimia 36.47 ya mwaka uliopita hadi asilimia 46.70 mwaka huu," alisema.

Naibu Waziri huyo alisema kuwa tofauti na mwaka jana, wahitimu wa mwaka huu wamefanya vizuri katika somo la Hisabati,  hivyo kuongeza kiwango cha ufaulu kutoka asilimia 24.70 hadi asilimia 39.36 mwaka huu.
Alisema katika somo la Sayansi ufaulu umekuwa hadi asilimia 61.33 kutoka asilimia 56.05 mwaka jana. Mulugo alisema viwango vya ufaulu kwa masomo ya Kiswahili na Maarifa ya Jamii vimeporomoka kutoka asilimia 71.02 hadi asilimia 68.58 kwa Kiswahili na kutoka asilimia 68.01 hadi 54.85 kwa Maarifa ya Jamii.
                                               Chanzo ni mwananchi

No comments:

Post a Comment

COMMENT HAPA UKIMALIZA, KWENYE PROFILE SELECT ANONYMOUS KISHA BONYEZA PUBLISH.