RAIS Jakaya Kikwete emesema licha ya kelele za wanasiasa, atasaini Sheria ya mchakato wa kuunda Katiba Mpya.
Alitoa kauli jana na kupangua hoja zote kupinga mchakato huo zilizotolewa na Chadema kwamba muswada huo haukuzingatia kanuni zitakazowezesha demokrasia.Kauli hiyo ya Rais imekuja saa chache baada ya Bunge kupitisha Muswada wa Mabadiliko ya Katiba ambao ulisusiwa na Wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi kwa madai kuwa mchakato mzima una kasoro.
Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dar es Salaam katika Ukumbi wa PTA, Sabasaba juu ya hali ya uchumi nchini na mchakato wa Katiba, Rais Kikwete alisema atatia saini sheria ya mchakato wa kuunda katiba mpya ambayo inatokana na muswada uliopitishwa na Bunge jana.
Alikibebesha lawama nyingi Chadema kwa kile alichosema ni upotoshaji wa mchakato huo kwa lengo la kuuvuruga wakati unaendeshwa kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi.
Alimtupia shutuma za waziwazi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akisema amekuwa kigeugeu kwa sababu mwanzo alimsifu (Rais Kikwete), kwa kukubali Katiba kubadilishwa lakini baadaye akageuka na kuanza kumponda.
“Mbowe ni miongoni mwa watu walionimwagia sifa baada ya kutangaza nia yangu ya kuanza kwa mchakato wa Katiba Mpya, nakumbuka ilikuwa Februari 11, mwaka huu wakati akichangia hotuba yangu katika Kikao cha Bunge alisema: ‘Tunampongeza Rais katika suala hili.’ Ila muda mfupi baadaye chama chake kikaja na mtizamo tofauti wa kunyang’anywa hoja yao… na kwamba Rais asiunde tume wala kuhusika katika mchakato.”
Alisema alishangazwa na kauli za Chadema na kusema: “Hii si mara ya kwanza kwa nchi yetu kufanya zoezi la marekebisho ya Katiba na hata kuandika Katiba Mpya.”
Alisema kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi, katika suala la upatikanaji wa Katiba anayeunda tume ni Rais na akisema hata katika utawala wa Awamu ya Kwanza na ya Pili, ilibadilishwa mara tatu na Rais ndiye aliyeunda tume.
“Mwaka 1977 yalifanyika mabadiliko mengine ya Katiba ambayo yalitengeneza Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ilikuja kufanyiwa marekebisho makubwa mwaka 1984,” alisema Rais Kikwete.
Mwaka 1991 na 1992, alisema iliundwa tume nyingine iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali ya kukusanya maoni ya Katiba ya kutoka mfumo wa chama kimoja kwenda vyama vingi.
“Tume hii ilipendekeza sheria 40 zifutwe, zilifutwa na nyingine zinaendelea kufutwa ikiwemo sheria ya kumweka mtu kizuizini,” alisema.
Alisema mwaka 1997 katika utawala wa Rais Benjamin Mkapa aliundwa Tume ya Jaji Kisanga ambayo ilikusanya maoni ya mabadiliko ya 13 na 14 ya Katiba.
“Siku zote katika mchakato wa Katiba, tume huundwa na Rais, sasa iweje sasa?... Rais amepungukiwa sifa kikatiba?” alisema na kusisitiza kwamba ndiye mwenye mamlaka kikatiba kuunda kamati hiyo.
Alisema iwapo Chadema kitaandaa mchakato wake wa kuunda katiba itabidi mawazo yao wayakabidhi kwa kamati atakayoiunda.
Alisema tayari CUF iliwasilisha rasimu yake ya Katiba na kuikabidhi serikalini na kwamba nayo itapelekwa kwenye kamati kama sehemu ya maoni yaliyotolewa na makundi ya Watanzania.
Rais alisema uteuzi wa wajumbe katika tume utazingatia sifa na kwa mujibu wa kanuni akisema hana mamlaka ya kuichagua kwa kuzingatia vigezo vya urafiki.
Isitoshe, alisema kitendo chake cha kuridhia mabadiliko ya Katiba nchini kwa sasa hakina maana kwamba iliyopo haifai. Alisema iliyopo imeiongoza vizuri nchi na kuwa kwenye utulivu na amani kwa miaka 50, hivyo haipaswi kuonekana kuwa haifai: “Lengo la kutaka mabadiliko hayo ya Katiba ni kuunda mpya itakayoendana na matakwa ya Watanzania katika wakati huu ambao wanatimiza miaka 50 tangu uhuru wao.”
Alisema Katiba itakayoundwa itajumuisha mawazo ya Watanzania wote ili kuhakikisha kuwa italiongoza vyema taifa katika miaka mingine 50 likiwa tulivu na lenye mshikamano.
Rais kuwa dikteta
Alisema kauli kuwa anaongoza kwa kutumia mtindo wa kidikteta ni za kizushi akisema endapo ingekuwa hivyo, angewatia kizuizini watu wengi ambao wanatoa hoja za kupotosha mambo yanayotendwa na Serikali yake.
Badala yake alisema amekuwa mvumilivu wa yote kwa kuwa anajua wazi katika nchi inayoongozwa kidemokrasia, lazima kuwepo na tofauti za mawazo. Alisema angekuwa hivyo, hata wanaomwita dikteta wasingethubutu kutamka hayo maana wangekamatwa na kutiwa kizuizini au kupotea katika mazingira utata.
Alikigeuzia kibao Chadema akisema kama ni udikteta basi ndicho chenye sifa hiyo kwa kuwa viongozi wake wamekuwa hawataki kuzingatia demokrasia kwa kulazimisha mambo.
Alisema kuwa amekuwa akishangazwa na kauli za Chadema akitoa mfano wa iliyotolewa na chama hicho kuwa kama Katiba mpya haitaandikwa kabla ya Uchaguzi Mkuu ujao 2015... “Patakuwa hapatoshi.”
Akasema lakini hata pale alipokubali mchakato wa kuunda katiba hiyo kabla ya mwaka 2015, ili ‘patoshe’ bado Chadema kimekuja na kauli nyingine mchakato huo ukiendelea kuwa “Patakuwa hapatoshi.”
Muswada wapita
Awali, jana mchana wakati kazi ya kupiga kura ikianza ili kupitisha muswada huo, wabunge wa Chadema na NCCR Mageuzi, hawakuwepo ndani ya Ukumbi wa Bunge kwa kwani walitoka muda mfupi baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu wakiendeleza msimamo wao wa kupinga muswada huo.Baada ya kuwahoji wabunge, Spika wa Bunge, Anne Makinda alisema: “Muswada umepita na sasa tunasubiri Rais aweke mkono wake ingawa wapo wanaosema aukatae sasa sijui wana maana gani...” alisema na kushangiliwa na wabunge.
Kabla ya kupitishwa, muswada huo ulifanyiwa marekebisho kadhaa yaliyotokana na hoja zilizotolewa na wabunge ambao waliitaka Serikali kuvifanyia marekebisho baadhi ya vifungu vyake.
Makinda aliwaponda wabunge waliosusia mjadala wa kupitishwa kwa muswada huo akisema kitendo hicho si cha kiungwana.
Alisema kulingana na nafasi zao, alitegemea kwamba wangehudhuria vikao hivyo na kutoa hoja mbadala ili wananchi wajue kile wanachokilalamikia.
“Nilitegemea kuwaona katika vikao ili watoe maoni yao kuhusu muswada huu na wapi palipokosewa kuliko kutoka nje. Sasa wananchi watajua sababu ya wao kususia jambo hili?”
Viongozi wa dini waonya
Wakati Bunge likipitisha Muswada wa Marekebisho ya Katiba jana, baadhi ya viongozi wa dini wameponda hatua hiyo wakisema Serikali haikuwatendea haki Watanzania kwa kuwa hatua hiyo imelazimishwa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana viongozi hao walisema Serikali ilipaswa kusikiliza hoja za wapinzani na wanaharakati waliotaka muswada huo usomwe bungeni kwa mara ya kwanza na siyo mara ya pili.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini alisema Serikali ilipaswa kufuatilia suala hilo kwa wananchi kabla ya kuupitisha muswada huo vinginevyo ilichofanya jana, ni kupitisha matakwa yake.
“Serikali haikutakiwa kuupitisha muswada huo kwa sababu wananchi hawajatoa maoni ya kutosha. Muswada huo ulipaswa kurejeshwa kwa wananchi ili watoe maoni yao ili katiba itakayotengezwa iwe inayojitosheleza,” alisema Askofu Kilaini.
Askofu Kilaini alisema Muswada wa Katiba Mpya, hauwezi kupitishwa kwa matakwa ya watu wachache akisema ni lazima wananchi washirikishwe.
Kauli ya Kilaini iliungwa mkono na Katibu wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Mchungaji Leonard Mtaita aliyesema kuwa mchakato huo ni jambo jema lakini, akaonya kwamba mgawanyiko uliojitokeza katika hatua za awali ni hatari.
“Kuwa na tofauti za kimtazamo katika jambo hili ni suala la kawaida, lakini mgawanyiko katika hatua hizi za awali ni hatari kwa taifa na unaweza kusababisha hata lengo lililokusudiwa kutofikiwa,” alisema Mtaita.
Alisema ni wajibu kwa Serikali kuhakikisha Watanzania wanadumisha umoja katika mchakato huu wa kuandika upya Katiba ya nchi ili malengo yaliyokusudiwa yafikiwe.
Mtaita alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutumia hekima zake katika kufanikisha jambo hilo kwa sababu muswada huo haupingwi tu na watu waliosusa kuhudhuria vikao bungeni, bali pia na makundi mengine ya watu wakiwamo wataalamu.
Alishauri Rais kuunganisha makundi hayo kwa kuwaleta karibu viongozi wastaafu na wanaharakati ili kupata muafaka wa Katiba Mpya.
Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alitaka Serikali kuzishirikisha kikamilifu taasisi za dini nchini katika mchakato huo ili watoe mchango wao katika kuwaelimisha waumini... “Kama taasisi za dini zitapewa nafasi kushiriki katika suala hili la Katiba, tunaweza kuisaidia Serikali kupata mawazo mazuri ambayo yatachangia kuleta Katiba itakayojitosheleza na itakayojenga umoja na kuleta maendeleo ya taifa.”
Sheikh Salum alisema baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakitumia fursa ya kuundwa Katiba Mpya kujitafutia umaarufu kisiasa akisema jambo hilo si jema kwa mustakabali wa taifa.
“Suala la uundwaji wa Katiba mpya ni muhimu. Linatakiwa kuangaliwa kwa umakini, sasa watu wanapoanza kutumia uundwaji wa katiba hiyo kujijenga kisiasa inaweza kuleta athari kubwa kwa taifa,” alisema.
Aliwataka wananchi kuheshimu Bunge kwa sababu ndicho chombo kinachotunga sheria za nchi badala ya kufanya uamuzi wa kishabiki na kusababisha kutoweka kwa amani ya nchi.