Pages

Sample Text

Frank Kimaro run this blog

11/26/2011

Aliyekuwa Jaji mkuu Mh. Augustino Ramadhani ahadhiri katika chuo kikuu cha Tumaini Iringa.

        Prf. Nicholas Bangu alipokuwa akimkaribisha Jaji mkuu kwa ajili ya kuongea na wanafunzi

                      Jaji mkuu akiwa anaelezea jambo wakati alipodhuru chuo kikuu cha Tumaini-Iringa

                       Baadhi ya wanafunzi walioudhuria katika mhadhara huo.

                                  Jaji mkuu akiwa anajadili kitu na mkuu wa chuo Prf. Nicholas Bangu


         Prf. Nicholas Bangu akiwa anamuuliza swali aliyekuwa jaji mkuu Augustino Ramadhani

                                 Jaji mkuu akiwa anajibu swali aliloulizwa na Prf. Bangu

Dk. Monica mhadhiri wa masomo ya sheria baada ya kumuuliza swali Jaji mkuu
                                          Wanafunzi wa sheria wakiwa wanamsikiliza Jaji mkuu


11/23/2011

Raisi amekubali kukutana na viongozi wa Chadema; ni katika mtanange mzima wa muswada wa katiba


RAIS Jakaya Kikwete amekubali kukutana na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema kusikiliza madai yao juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, uliopitishwa bungeni juma lililopita.Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu jana jioni ilieleza kuwa Rais amelipokea ombi hilo kwa furaha kwa sababu ni jambo jema.

“Kufuatia kukubali kwake ombi hilo, Rais ameagiza mawasiliano yafanyike ili kupanga tarehe mwafaka ya kukutana na viongozi hao wa Chadema na kuzungumzia suala hilo,” ilieleza taarifa hiyo.

Kabla ya Kurugenzi hiyo kutoa taarifa hiyo, Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga akizungumza na gazeti dada la hili, The Citizen alisema Rais amepokea jambo hilo kwa furaha.

“Tumepokea barua ya Chadema muda mfupi uliopita (jana jioni), ikiomba kukutana na Rais Kikwete na bahati njema Rais pia amependekeza kuwa yuko tayari kukutana na viongozi kutoka vyama vya siasa,” alisema Kibanga.

Uamuzi huo wa Rais umekuja siku moja baada ya Chadema kuunda kamati ndogo ya watu sita kwa ajili ya kuonana na Rais Kikwete na kuwasilisha madai yake juu ya muswada huo wa sheria.

Kamati hiyo iliyoundwa katika mkutano wa dharura wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, inataka kujadiliana na Rais kuhusu kile ilichoeleza kuwa ni upungufu uliopo katika muswada huo uliopitishwa na Bunge na kutaka Rais atafakari kama ausaini kuwa sheria au la.

Akisoma tamko hilo kwa vyombo vya habari katika mkutano uliofanyika makao makuu ya chama hicho, Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema kamati hiyo ya watu sita, ilikuwa ikifanya taratibu za kumuona Rais Kikwete.

Mbowe alisema ushiriki wa Chadema katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya utategemea mazungumzo hayo baina ya wajumbe wa kamati ya chama chake na Rais Kikwete.

Ijumaa iliyopita, Rais Kikwete akizungumza na wazee wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam kuhusu uchumi na mchakato wa Katiba, alisema atautia saini kuwa sheria muswada huo licha ya kelele za wanasiasa za kuupinga.

Alitoa kauli hiyo huku akipangua hoja zote kuhusu mchakato huo zilizokuwa zikitolewa na Chadema kuwa muswada huo haukuzingatia kanuni zitakazowezesha demokrasia.

Kauli hiyo ya Rais ilikuja saa chache baada ya Bunge kupitisha muswada wa mabadiliko ya Katiba ambao ulisusiwa na wabunge wa Chadema na NCCR-Mageuzi kwa madai kuwa mchakato mzima una kasoro.

Kamati Kuu CCM bado siri nzito

Huko Dodoma, ajenda kuhusu Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), ilijitokeza kwa sura isiyo rasmi wakati Kamati Kuu (CC), ilipokuwa ikijadili taarifa ya uchaguzi mdogo wa Igunga iliyowasilishwa na aliyekuwa Kiongozi wa Kampeni za CCM, Mwigulu Nchemba lakini haikudumu.

Habari kutoka katika kikao hicho zinasema mmoja wa wajumbe wa CC ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi akichangia hoja ya uchaguzi wa Igunga alisema hali ya vijana wa jimbo hilo na kwingineko nchini kukichukia CCM ni kutokana na Umoja wa vijana kutotekeleza wajibu wake, badala yake kujishughulisha na mambo mengine yasiyokuwa na tija.

Lukuvi ambaye pia ni Mbunge wa Isimani, Iringa alinukuliwa akitoa kauli hiyo baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira kusema kuwa tatizo katika uchaguzi mdogo wa Igunga walikuwa ni vijana wengi ambao walionyesha chuki kwa CCM wakati wa uchaguzi huo, wakidai kutoshughulikiwa kwa matatizo yao.

Uchaguzi Igunga
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zimeeleza kuwa katika siku ya kwanza ya kikao chake juzi, CC ilipokea taarifa ya uchaguzi mdogo wa Igunga ambao ulimwingiza bungeni, Dk Dalaly Kafumu.

Ripoti ya Igunga iliyowasilishwa na Nchemba iliweka bayana kwamba hali katika uchaguzi huo ilikuwa mbaya kiasi cha kuwepo kwa hofu ya CCM kushindwa uchaguzi.

Nchemba alinukuliwa akieleza mitafaruku kadhaa iliyotokea wakati wa kampeni kiasi cha kuwafanya madiwani wa CCM Igunga kutishia kujitoa katika chama na kuingia upinzani, lakini akasema suala hilo lilimalizwa kwa kutumia busara, hatua iliyokiwezesha kupata ushindi.

Baada ya taarifa ya Mwigulu, Mwenyekiti wa kikao hicho, Rais KIkwete anadaiwa kwamba alihoji ukweli wa taarifa za baadhi ya makada wa chama hicho kuwapigia kampeni wapinzani kwa kutumia kauli mbiu ya “Tushindwe ili tuheshimiane”, swali ambalo hata hivyo, halikupata majibu kutokana na wajumbe kukaa kimya.

“Mwenyekiti aliuliza tena kwamba kuna watu waliompigia simu na kumtumia meseji (ujumbe mfupi wa simu wa maandishi), kwamba kuna makada waliokuwa wakiwapigia kampeni Chadema, lakini wote walikaa kimya na ndipo aliposema kwamba tuache majungu na fitina,” kilisema chanzo chetu kutoka ndani ya mkutano huo.
                                                     Chanzo ni mwananchi

11/22/2011

Harakati zinaendelea Chadema yaunda kamati ya kukutana na Kikwete.

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeunda kamati ndogo ya watu sita kwa ajili ya kwenda kuonana na Rais Jakaya Kikwete kuwasilisha madai yake juu ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba wa mwaka 2011, uliopitishwa bungeni juma lililopita.

Kamati hiyo imeundwa katika mkutano wa dharura wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, uliofanyika Dar es Salaam juzi ili kukutana na Rais Kikwete kumjulisha kile walichoeleza kuwa upungufu wa muswada huo na kisha kumtaka atafakari kama ausaini kuwa sheria au la.

Akisoma tamko hilo kwa vyombo vya habari katika mkutano uliofanyika Makao Makuu ya Chadema jana, Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe alisema kamati hiyo ya watu sita, inafanya taratibu za kumuona Rais Kikwete wakati wowote kuanzia sasa.

Mbowe alisema kamati hiyo itaongozwa na yeye, Katibu Mkuu Dk Willbrod Slaa, Makamu Mwenyekiti (Bara) Said Arfi na Makamu Mwenyekiti (Zanzibar), Said Issa Mohamed. Wengine ni Mshauri wa Masuala ya Siasa wa chama hicho, Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye pia atakuwa katibu wa kamati hiyo wakati wa mkutano huo.“Hivi sasa taratibu za kumuona Rais zinaendelea, tutamuona wakati wowote kuanzia sasa na kumweleza mapendekezo yetu juu ya upungufu uliomo kwenye muswada wa sheria hiyo na kama atatusikiliza tutashirikiana naye akikataa tutawaeleza wananchi hatua za kuchukua,” alisema Mbowe.

Alisema ushiriki wa Chadema katika mchakato wa kuandika Katiba Mpya utategemea mazungumzo hayo akisema hiyo ndiyo fursa pekee inayoweza kutumika licha ya muswada huo kupitishwa ‘kibabe’.

“Bado kuna fursa za kisiasa na kijamii katika kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya haja ya nia na mchakato na misingi ya Katiba Mpya, Kamati Kuu imesikitishwa na uamuzi wa Rais Jakaya Kikwete badala ya kuzitumia fursa hizo amejiingiza kwenye upotoshaji uliofanywa na wabunge wa chama chake juu ya misingi na maudhui ya sheria hiyo,” alisema Mbowe na kuongeza,

“Kamati Kuu inaamini badala ya kuwaunganisha Watanzania na kujenga muafaka wa kitaifa unaohitajika katika kuandika Katiba Mpya, hotuba ya Rais Kikwete kwa wazee wa CCM wa Mkoa wa Dar es Salaam imezidi kuwagawa wa Tanzania kwa misingi ya ushabiki wa vyama vya siasa kitendo hiki ni hatari kwa Taifa.”

Alisema Katiba si mali ya viongozi wala wanasiasa, bali ni ya wananchi inayohitaji mchango mpana wa maoni yao juu ya kuunda sheria itakayokusanya maoni na hata kuundikwa kwake.

Alisema Chadema kitaendelea kuwaelimisha wananchi na wadau wote juu ya ubovu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na umuhimu wa kuwa na sheria bora itakayoratibu uundwaji wa tume ya kukusanya maoni.
Chama hicho kimewaagiza wabunge na viongozi wake kufanya mikutano ya ndani na ya hadhara yenye lengo la kuwaelimisha wananchi juu ya sheria hiyo na madhara yake.

Yalia na Polisi

Kamati Kuu ya Chadema pia imelaani kitendo cha Serikali kukizuia chama hicho kufanya mikutano na maandamano nchi nzima kwa kile ilichodai ni kukinyima haki ya kikatiba ya kufanya shughuli zake.

“Polisi kuzuia mikutano ya hadhara ya Chadema na maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga mchakato uliopitishwa kuwa  sheria siyo tu kwenda kinyume na haki za msingi za kikatiba, bali pia unahatarisha amani na utulivu wa nchi,” alisema Mbowe.

Aliitaka Serikali kutoa tamko la kufuta amri hiyo huku akisisitiza kuwa Chadema kitaendelea kutumia njia zote za amani zilizopo ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano kama ilivyoainishwa katika Katiba ya sasa.

Kwa nini waligoma?
Awali, Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alitaja sababu saba zilizowafanywa wasusie mjadala huo ikiwamo kukiukwa kwa Kanuni za Kudumu za Bunge wakati wa uwasilishwaji muswada huo.

Alisema Kamati ya Bunge iliingiliwa kazi zake kwa kuzuiliwa kukusanya maoni katika kanda 10 kama ilivyokuwa imepanga na badala yake maoni yakakusanywa kinyume na utaratibu na kuingizwa kwenye muswada huo.
Aliishutumu Serikali akidai kuwa iliingilia mchakato huo kwa kumtumia Spika wa Bunge, Anne Makinda.

Akizungumzia hatua ya wabunge hao kususa, Dk Slaa alisema kamati ilipongeza hatua hiyo akisema ulikuwa uamuzi wa kijasiri uliowafanywa wasiwe sehemu ya kupitishwa sheria mbovu.

“Kamati Kuu imewapongeza wabunge wa Chadema kwa kususia vikao vya kupitisha sheria hiyo kwani ushiriki wao ungeipa uhalali wa kisiasa na kijamii, sheria ambayo haikuzingatia nia ya haja ya dhati ya kuweka utaratibu wa kisheria utakaoiwezesha nchi yetu kupata Katiba Mpya,” alisema.

Wabunge wa Chadema na wenzao wa NCCR-Mageuzi, walisusia kikao cha Bunge kilichojadili na kupitisha Muswada wa Sheria mpya ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.

                                                  chanzo ni mwananchi