Pages

Sample Text

Frank Kimaro run this blog

11/18/2011

Wanaharakati wasema endapo katiba itasomwa maandamano yatafanyika nchi nzima.


  • Wanaharakati wageuka mbogo,watoa onyo kali
  • Watishia kuitisha maandamano yasiyo na kikomo
  • Ni endapo Muswada wa Katiba utasomwa leo
  • Wasema hakuna polisi, mgambo atakayewauzia
Akizungumza wakati wa kuhitimisha mjadala wa Katiba uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba, alisema njia pekee ya kuepusha maandamano hayo ni Serikali kusoma Muswada huo kwa mara ya kwanza na si mara ya pili kama ambavyo imekwishatangaza.
“Napenda kuwaambia ndugu washiriki kama kesho (leo), Serikali itasoma Muswada huu kwa mara ya pili, tutaitisha maandamano ya nchi nzima yasiyokuwa na kikomo.
“Tarehe na siku tutawaambia muda si mrefu, tunataka kuona muswada huu unasomwa kwa mara ya kwanza ili Watanzania wapate fursa ya kuujadili,”alisema Kibamba na kupigiwa makofi.
Alisema Jukwaa la Katiba litaongoza maandamano hayo, ambayo lengo lake ni kupinga jeuri ya Serikali.
“Inasikitisha kuona viongozi wa Tanzania ni waoga mno, nawahakikishia kwamba  maandamano ya katiba yatatisha, hatuogopi  polisi, mgambo wala  wanasiasa watakaozuia dhamira yetu,”alisema Kibamba.
Wakichangia kongamano hilo kwa nyakati tofauti, wanaharakati na washiriki wa mjadala huo, walisema viongozi  hawajifunzi wala kuonyesha uzalendo, zaidi ya kujadili posho na marupurupu, huku wakishindwa kuwatetea wananchi.
“Wabunge waache kushabikia Serikali ya kikoloni, tunataka waitetee Tanzania, sisi ndio tunaowapa mamlaka ya kwenda mjengoni (bungeni), kama kesho (leo) watausoma Muswada huu kwa mara ya pili, tutadai haki yetu barabarani bila kuogopa chochote,
“Tutakapofanya maandamano hatutahitaji polisi, zile bunduki na mabomu ya machozi na maji ya kuwasha, wakawapigie mafisadi ambao wanatumia fedha za walipa kodi kwa maslahi yao,”alisema Paulina Makuli.
Naye  Renatus Pamba, alisema wingi wa wabunge wa Chama Cha Mapinduzi(CCM), unatia wasiwasi kwani huenda kukawa na kura nyingi za kutaka kupitisha Muswada huo usomwe mara ya pili kwa maslahi binafsi.
Alisema kamwe hawataogopa kudai haki yao, kwani miaka 50 ya kuburuzwa na hali ngumu ya maisha  imefikia kikomo.
“Tunawashangaa sana hawa viongozi wetu, mbona wanapokuja kuomba kura hawatwambii sisi walemavu tusiwapigie, ndiyo kwanza wanakusogeza karibu na kukuonyesha majina ya viongozi na vyama vyao, kwa nini wakati wa kuandika Muswada huu hawakutuwekea mazingira rafiki katika usomaji, au sisi siyo Watanzania, ”alihoji mmoja wa wanaharakati hao, Maria Charles.
…Tunawaomba viongozi wetu watutambue makundi maalum katika uandishi wa muswada  huo kwa kutumia nukta nundu ili na sisi pia  tuweze kusoma bila kuhitaji msaada wa mtu yeyote,”alisema
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Katiba mpya, unatarajiwa kusomwa kwa mara ya pili na tatu bungeni leo huku wananchi na wanaharakati wakizidi kuupinga.

No comments:

Post a Comment

COMMENT HAPA UKIMALIZA, KWENYE PROFILE SELECT ANONYMOUS KISHA BONYEZA PUBLISH.