Pages

Sample Text

Frank Kimaro run this blog

12/13/2012

Ponda afikishwa tena mahakamani: Mashahidi wawili wasikilizwa


                                  Akiwa anasindikizwa na ulinzi wa maaskari kuelekea mahakamani


                                             Ulinzi ukiwa umeimarika vyema

Na Flora Mwakasala
MJUMBE wa Baraza la Ulamaa, Shekhe Habibu Ismail (46) ameieleza mahakama kuwa baraza hilo liliridhia na kutoa kibali kwa Baraza la waislamu Tanzania (Bakwata) kubadilishana ardhi na na kampuni ya AgriTanza.
Alidaa hayo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam wakati akitoa ushahidi katika kesi ya uchochezi na wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59 inayomkabili Katibu wa Jumuiya ya Waislamu Shekhe Ponda Issa Ponda na wenzake 49.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali Tumaini Kweka kutoa ushahidi, Shekhe Ismail alidai kuwa, kampuni hiyo inamiliki kihalali kiwanja kilichopo katika eneo la Chang’ombe markazi kwa kuwa walifuata taratibu zote za kubadilishana ardhi.
Alidai kuwa Januari 3 mwaka jana baraza hilo lilikaa kikao na kutoa majukumu kwa Katibu wa Bakwata pamoja na timu yake yautendaji kutafuta eneo kubwa kwaajili ya ujenzi wa Chuo Kikuu cha Kiislamu ambapo Januari 8 walisema wamepata eneo la ekari 40.
Shekhe Ismail ambaye ni Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga alidai kuwa, walikwenda kuliona eneo hilo lililopo Kisarawe Mkoani Pwani, kwa kuwa walikuwa na wasiwasi kutokana na eneo lao kuwa ekeri nne na kampuni hiyo kukubali kuwapa ekari 40.
Akihojiwa na wakili wa washitakiwa, Juma Nassoro, Shekhe Ismail alidai kuwa hafahamu utaratibu uliotumika kuipata kampuni ya Agritanza kwa kuwa watendaji wakuu walikuwa Bakwata na hajui kwanini eneo hilo ambalo awali alidai lilikuwa ni ekari 27 lilibaki ekari nne.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kampuni ya Agritanza, Suleiman Mohamed akitoa ushahidi alidai kuwa alisikia Bakwata wanatafuta eneo la ekari 30 na wapo tayari kubalishana ndipo walipoamua kuwatafuta na wakaambiwa watakubaliana baada ya kufuata taratibu.
Alidai baada ya kupata eneo hilo walizungusha ukuta kutenganisha eneo lao na shule ya kiislamu ya markazi lakini aliambiwa Ponda na wenzake walifika hapo na kuwaamuru mafundi wasimamishe ujenzi na wao waliafiki lakini baada ya muda  watu wanaokadiriwa kuwa zaidi 300 walivamia eneo hilo na kuanza ujenzi.
Hata hivyo akihojiwa, Mohamed alidai hawafahamu washitakiwa hao na kwamara ya kwanza alimuona Ponda alipokwenda kutoa maelezo kituo cha polisi na kuongeza kuwa hakuibiwa mali zake lakini watu asio wafahamu walitumia matofali mchanga na kokoto kujenga.
Mahakama imepokea vielelezo vitatu ambavyo Muhutasari wa kikao cha Januari 3 na Januari 8 mwaka jana cha Baraza la Ulamaa pamoja na mkataba baina ya Bakwata na Kampuni ya Agritanza. Kesi itatajwa tena desemba 18 na kuendelea kusikilizwa desemba 31 mwaka huu.
                                      Polisi wakiwalinda wafuasi wa Ponda

                                 Wakili wa Ponda Bw Juma Nasoro akiongea na wafuasi wa Ponda

No comments:

Post a Comment

COMMENT HAPA UKIMALIZA, KWENYE PROFILE SELECT ANONYMOUS KISHA BONYEZA PUBLISH.