Pages

Sample Text

Frank Kimaro run this blog

12/12/2011

Dk. Mwakyembe arejea nchini


NAIBU Waziri wa  Ujenzi na Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe, amerejea nchini akitokea Hospitali ya Apollo nchini India alikolazwa kwa ajili ya matibabu ya ugonjwa wa ngozi.  Dk Mwakymbe aliondoka nchini Oktoba 9 mwaka huu kwenda nchini India baada ya hali yake ya afya kuzorota huku ngozi yake ikionekana kudhoofika.

Baada ya kukaa India kwa takriban miezi miwili, jana saa 7:00 mchana, Dk Mwakyembe aliwasili nchini kupitia Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius Nyerere kwa ndege ya Shirika la Qatar Airways.

Habari zilizolifikia gazeti hili jana mchana zilieleza kuwa baada ya kutua jijini Dar es Salaam, Dk Mwakyembe aliondoka moja kwa moja kuelekea mkoani Mbeya.  Akizungumza na gazeti hili jijini Dar es Salaam jana, Msemaji wa Familia na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa alisema, afya ya mbunge huyo wa Kyela, ni nzuri ndio maana ameruhusiwa kutoka hospitali.

  “Ni kweli Dk Mwakyembe amerejea nchini salama .Tunamshukuru Mungu, hii inatokana na madaktari waliokuwa wakimpatia matibabu kumpa ruhusa baada ya kuona hali yake ni nzuri na kwamba anaweza kuendelea na majukumu yake kama kawaida,” alifafanua Mwambalaswa na kuongeza:

“Kutokana na hali hiyo, tunaamini kuwa, kurudi kwake nchini, kutaleta matumaini mapya ya afya yake.”  Msemaji huyo wa familia alisema, baada ya kurudi, Dk Mwakyembe atapumzika kijijini kwao Kyela ili aweze kujumuika na wanafamilia katika kipindi hiki cha Sikukuu ya Chrismasi na mwaka mpya, kabla ya kuanza kazi rasmi ya ujenzi wa taifa mwakani.

Alisema, kutokana na hali hiyo anaamini, sala za wananchi ni miongoni mwa mambo yaliyofanya apone haraka na kurudi nyumbani Kuugua
Taarifa za kuugua kwa Dk Mwakyembe zilianza kuvuma mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka huu baada ya kuanza kupata matibabu nchini.

Hata hivyo, kutokana na afya yake kuendelea kuzorota,  Serikali ililazimika kumkimbiza nchini India kwa ajili ya matibabu zaidi.

Taarifa za awali, zilisema Dk Mwakyembe alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari ambapo alikuwa akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Lakini, taarifa hizo za ugonjwa wa kisukari zilipingwa na baadhi ya washirika wake wa karibu kisiasa,  ambao waliamini  Naibu waziri huyo, alilishwa sumu iliyosababisha nywele zake kunyonyoka, ngozi ya mwili wake kupepetuka na kutoa unga, huku akiwa amevimba. Hata hivyio ilielezwa kuwa, madaktari nchini India ndio pekee ambao wangeweza kuangalia namna ya kumsaidia katika ugonjwa huo.

No comments:

Post a Comment

COMMENT HAPA UKIMALIZA, KWENYE PROFILE SELECT ANONYMOUS KISHA BONYEZA PUBLISH.